Friday, October 12, 2012

Taarifa kwa UmmaKUKAMILIKA MAANDALIZI YA KONGAMANO LA KWANZA LA AFRIKA KUHUSU USIMAMIZI WA UTALII ENDELEVU KATIKA HIFADHI
(Ilitolewa mbele ya Waandishi wa Habari Dar es Salaam tarehe 10 Oktoba 2012)
Nimewaiteni hapa leo kuwajulisha kuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Mohamed Ghalib Bilal atakuwa Mgeni Rasmi katika ufunguzi wa ‘Kongamano la Kwanza la Afrika kuhusu Usimamizi wa Utalii endelevu katika Hifadhi za Taifa’ ambao utafanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Arusha (AICC) kuanzia tarehe 15 hadi 18 Oktoba 2012.
Wizara ya Maliasili na Utalii imeandaa Kongamano hilo kwa kushirikiana na Shirika la Utalii Duniani (UNWTO) na Kamati ya kitaifa iliyoundwa na Wizara.
Jumla ya watu 412 kutoka nchi 40 za Afrika walisajili ushiriki wao kabla ya siku ya mwisho ya usajili, tarehe 5 Oktoba 2012. Kati yao washiriki 242 (yaani asilimia 59) watatoka Tanzania na washiriki 170 (asilimia 41) wanatoka nchi zingine za Afrika.
Washiriki hao ni pamoja na Mawaziri 12 kutoka Bara la Afrika ambao watawakilisha nchi za Cameroon, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Guinea, Mali, Mauritania, Mozambique, Namibia, Niger, Seychelles, Sierra Leone, Tanzania na Uganda.
Aidha, Kongamano hilo litahudhuriwa na wajumbe 6 kutoka UNWTO ambao wataongozwa na Katibu Mkuu wa shirika hilo Bw. Taleb Rifai.
Tanzania iliteuliwa kuwa mwenyeji wa Kongamano hilo na Shirika la Umoja wa Mataifa la Utalii Duniani (UNWTO) kufuatia mkutano wake (UNWTO General Assembly) ambao ulifanyika nchini Korea mwaka jana. Katika Mkutano huo Tanzania pia ilichaguliwa kuwa mjumbe katika Baraza la Utendaji (Executive Council) la Shirika hilo, nafasi ambayo itakuwa nayo hadi mwaka 2015. Kongamano la Arusha ni matokeo ya awali ya nchi yetu kushika nafasi hizo za UNWTO.
Katika Kongamano lijalo la Arusha Tanzania imepewa nafasi ya kuwasilisha mada tatu zitakazohusu uhifadhi unavyofanikisha utalii. Mada hizo zitatolewa na Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA), Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro, na Hifadhi za Bahari na Maeneo Tengefu (Marine Parks and Reserve Unit).
Aidha, katika siku zote za Kongamano kutakuwepo na maonesho ya wadau watakayonadi bidhaa za asili ambazo hutengenezwa kwa mikono hapa nchini. Maonesho hayo ya wadau ambayo yamepewa jina la Tangaza Bidhaa Zinazotengenezwa Tanzania (Showcase Made in Tanzania Products) yameandaliwa na Wizara kwa kushirikiana na Sekta Binafsi, yaani Tanzania Private Sector Foundation - TPSF.

Mwisho, ningependa kuwajulisha kuwa tarehe 18 Oktoba imetengwa maalum kwa wageni watakaopenda kutembelea maeneo yenye vivutio vya utalii, kama vile Hifadhi ya Ngorongoro.
Ahsanteni kwa kunisikiliza.

Mhe. Lazaro S. Nyalandu
NAIBU WAZIRI
WIZARA YA MALIASILI NA UTALII
10 Oktoba, 2012

No comments:

Post a Comment